
Watoto watano wa familia moja katika Kijiji cha Nyakanazi Kata ya Rusahunga Wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera wamefariki dunia kwa kile kinachosadikika wamekula chakula chenye sumu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema kuwa vimetokea kwa nyakati tofauti baada ya wanafamilia 11 kula chakula cha usiku Novemba 13, 2023.
Chatanda amesema, wanafamilia hao baada ya kula chakula cha usiku walikwenda kupumzika lakini asubuhi yake watoto watatu walianza kujisikia vibaya na kupelekwa Kituo cha Afya, Nyakanazi ambapo wakati wanaendelea na matibabu Novemba 14, 2023 walifariki dunia.
Amesema kuwa, baada ya watatu hao kufariki, watatu wengine walianza kujisikia vibaya na walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Biharamlo wakati wakiendelea na matibabu Novemba 15, 2023 nao walipoteza maisha na hivyo idadi ya waliofariki kuwa watano.
Aidha, amesema wanafamilia wengine ambao walishiriki chakula hicho akiwemo mama aliyepika wako salama na uchunguzi wa awali umebaini kuwa chakula kilikuwa na sumu na uchunguzi unaendelea kubaini ilikuwa ni sumu ya aina gani.