Watoto 600,000 Kupatiwa Chanjo Ya Polio Gaza

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA Phillipe Lazzarini amesema awamu ya kwanza ya zoezi kubwa la kampeni ya utoaji chanjo ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 limeanza rasmi Septemba Mosi huko katikati mwa ukanda wa Gaza, huku akieleza kuwa kampeni hii inakimbizana na muda ili iweze kufikia watoto 600,000 katika ukanda huo.

Katika taarifa yake aliyoichapishwa kwenye mtandao wa X Septemba 1,2024, Lazzarini amesema mama mmoja amemueleza anahisi ahueni baada ya mtoto wake kupata matone mawili ya dozi ya chanjo ya polio katika kliniki ya UNRWA.

Hata hivyo kiongozi huyo wa UNRWA amesisitiza kuwa ili kampeni hiyo iweze kufanikiwa, pande zote katika mzozo unaoendelea huko Gaza ni lazima ziheshimu sitisho la muda la mapigano katika ukanda huo.

“Kwa ajili ya watoto wa ukanda huu, ni wakati wa kuwa na sitisho la kudumu la mapigano,” aliongeza Lazzarini.

Kwa upande wake, Sam Rose, Kaimu Mkurugenzi wa Operesheni za UNRWA huko Gaza, kupitia chapisho kwenye mtandao wa X ameeleza kwamba, timu za mawakala zitawafikia maelfu ya watoto na kuwapatia chanjo ya polio katika kliniki, vituo vya afya na kupita kutoka hema hadi hema katika Ukanda mzima.

Amesisitiza kuwa UNRWA itatoa chanjo hadi kwa nusu ya watoto hao, na takriban wafanyakazi 1,100 wa shirika hilo watashiriki katika kampeni hiyo inayofanywa na Wizara ya Afya ya Palestina kwa ushirikiano na UNRWA, WHO na UNICEF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *