Takwimu Zinaonyesha Watoto 11, 000 Hadi 14, 000 Wanazaliwa Nchini Wakiwa Na Changamoto Ya Selimundu (Sickle Cell) Huku Asilimia Saba Ya Vifo Vya Watoto Chini Ya Miaka Mitano Vinatokana Na Changamoto Ya Ugonjwa Huo.
Hayo, Yamesemwa Na Mganga Mkuu Wa Serikali Profesa Tumani Nagu Katika Kongamano La Kisayansi Lililoandaliwa Na Chuo Cha Afya Na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) La Kujadili Mbinu Ambazo Zitaweza Kupunguza Tatizo La Ugonjwa Wa Selimundu Na Uzinduzi Wa Jarida Rasmi La Selimundu La Lancet.
Amesema Takwimu Hizi Zinaifanya Tanzania Kuwa Nchi Ya Tano Duniani Kwa Kuwa Na Wingi Wa Wagonjwa Wa Selimundu Na Kuwa Ya Tatu Katika Bara La Afrika.
Pia, Amesema Katika Vifo Vyote Vya Watoto Chini Ya Miaka Mitano Ugonjwa Wa Selimundu Husababisha Vifo 15,000 Kila Mwaka Sawa Na Asilimia Saba Ya Vifo Vyote Vya Watoto.
Aidha, Kutokana Na Changamoto Hizo Prof. Nagu Amebainisha Kuwa Serikali Imeendelea Kuchukua Hatua Za Makusudi Katika Kukabiliana Na Ugonjwa Huo Ambao Umekua Na Athari Kubwa Katika Jamii Ikiwemo Kutoa Muongozo Wa Matibabu Ya Selimundu Nchini.
Amesema, Muongozo Huo Unaainisha Nyanja Zote Kuanzia Kupunguza Tatizo Hilo Kwa Kufanya Utambuzi Wa Watoto Wachanga Na Uhakika Wa Matibabu.
Aidha, Muongozo Huo Unaelekeza Kufanyika Vipimo Vya Vinasaba Kwa Wachumba Kabla Ya Kuoana Ili Kupunguza Uwezekano Wa Kupata Watoto Wenye Selimundu.
Ameeleza Kuwa Muongozo Huo Unalenga Kufanya Utambuzi Kwa Watoto Zaidi Ya Milioni Mbili Wanaozaliwa Kila Mwaka Na Kuhakikisha Wanapata Matibabu Mapema Ikiwemo Chanjo, Dawa Za Antibiotiki Ili Wasipate Changamoto Zitokanazo Na Selimundu.