Na Gideon Gregory – Dodoma.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuwa na utamaduni wa kuwatembelea wakulima mashambani ili waweze kutambua changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Waziri Bashe ameyasema hayo Jijini Dodoma kwenye hafla utiaji saini makubaliano na Wakurugenzi wa Halmashauri 19 nchini juu ya usimamizi, uendeshaji na matunzo ya skimu za umwagiliaji, kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Vyama vya Umwagiliaji kupitia mradi wa mifumo himilivu ya Chakula Tanzania.
“Kuna uwezekano mkubwa kabisa msimu wa kilimo umeanza kuna Mkurugenzi hajaenda na kumwambia mwaka jana ulilima heka moja ulipata gunia ngapi, mwaka huu vipi ulipata changamoto zipi, ulipata matatizo gani hivi ndivyo vitu tunapaswa kuvijua ili tuweze kuwasaidia wakulima wetu kuondokana na changamoto wanazokabiliana nazo,” amesema.
Aidha amemtaka Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji kuwaandikia Wakurugenzi wote nchini barua za kuwaeleza mradi unaotekelezwa kwenye maeneo yao kwa fedha za bajeti pamoja na mradi unaotekelezwa kwa fedha za PforR na wawafanye mameneja wa Wilaya na Mikoa waripoti kila maradi unaofanywa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amesema serikali ilipata fedha za mkopo nafuu dola milioni 300 kwa ajili ya kutekeleza mradi katika kipindi cha miaka mitano.
Amesema, mradi huo utaenda kurekebisha maneo ya kilimo ili kuhakikisha skimu za wakulima zinawekewa mifumo sahihi kwa ajili ya uzalishaji.
Naye Mratibu wa Mradi huo Mhandisi Naomi Mcharo amesema mradi huo utatekelezwa nchi nzima ambapo kupitia sekta ya umwagiliaji mradi huo utagharamiwa kwa dola za kimarekani milioni na utaboresha mfumo wa mashirikiano kati ya tume na wakurugenzi wa Halmashauri.
“Tumeanza na wakurugenzi kutoka halmashauri 19 kutoka katika mikoa sita ambayo inalima sana kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ili kuwajengea uwezo wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa idara za kilimo ili tuweze kufanya kwa Pamoja utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi lakini matunzo na uendeshaji wa miundombinu imekuwa ni changamoto ndio maana tume ikaona ishirikiane na halmashauri za wilaya ili kurahisisha utunzaji wa skimu za umwagiliaji.
Mhandisi Naomi amesisitiza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani uwekezaji mkubwa umefanyika katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji ikiwemo ongezeko la bajeti kwa asilimia 300.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali Steven Katemba amesema mradi huo utasaidi kuongeza uzalishaji kwa wakulima wadogo.