Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati leo tarehe 18.12.2024 amewasimamisha kazi watoa huduma watatu wa Kituo cha Afya Magugu (Afisa tabibu, Afisa Muuguzi msaidizi na mteknolojia wa dawa) kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ya kazi.
Mkurugenzi huyo amechukua hatua hiyo baada yakupokea taarifa kupitia mitandao ya kijamii ikionyesha wanafamilia wakielezea namna ambavyo tukio la mwanamke mmoja ajulikanaye kwa jina la Juliana Obedi (43) aliyeng’atwa na nyoka na kufariki dunia baada ya kufikishwa kwenye Kituo cha Afya Magugu na kucheleweshwa kupata matibabu kwa tuhuma za kukosa shilingi Laki moja na nusu kwa ajili ya kugharamia matibabu hayo.
Mkurugenzi amesema pamoja na changamoto iliyojitokeza ya mgonjwa huyo kucheleweshwa kufikishwa katika kituo cha Afya masaa takribani sita baada ya kung’atwa na nyoka, huku mkono wa kulia aliong’atwa ukiwa umevimba na kubadilika rangi ikiashiria tayari sumu ilikuwa imemuathiri sana mama huyo, wataalam hao wa Afya walipaswa kumpatia kwanza mgonjwa huduma zote stahiki kwa dharura na masuala ya malipo yangekamilishwa baadae.