Na Pascal Tuliano – Tabora.
Watu watatu wamejeruhiwa baada ya Lori la Mizigo kugonga Treni katika mtaa wa miemba uliopo Kata ya Mbugani Manispaa ya Tabora.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao amesema Treni hiyo ya Abiria ilikuwa ikitoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam ambapo hakuna Kifo katika tukio Hilo.

“Ni kweli ajali hiyo imetokea eneo la miemba na imehusisha treni ya abiria ilivyokuwa inatoka Kigoma kwenda Dar Es Salaam, lakini hadi Sasa hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza katika ajali hiyo.” Amesema Kamanda Abwao.
Jambo Fm imefanikiwa kuzungumza na Dereva wa Lori hilo ambapo ameeleza kuwa wakati anakaribia eneo la makutano ya reli na barabara hakusikia honi ya treni na ghafla akajikuta gari inaburuzwa na treni hiyo ya abiria.

“Kiukweli Mimi sikusikia chochote, ghafla tu nikajikuta gari yangu imeshavamiwa na treni kisha tukaanza kuburuzwa mpaka upande huu.”
Nao mashuhuda wa ajali hiyo katika mtaa huo wa miemba wameieleza Jambo Fm kuwa walisikia treni ikipiga honi ya tahadhari na ghafla wakashuhudia lori likiburuzwa na treni kutoka katika makutano ya reli na barabara iendayo Kigoma.

“Mimi nilisikia treni ikipiga honi kama ilivyozoeleka inapokaribia maeneo kama haya, lakini nahisi dereva wa lori hakuwa makini maana hakupunguza mwendo wala kusimama. Nikaona lori linaburuzwa kutoka kwenye reli.” Amesema shuhuda mmoja.