Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameanzisha nafasi ya Naibu Waziri Mkuu na kufanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri na makatibu wakuu wa wizara.
Aliyekuwa waziri wa Madini, Dotto Biteko ndiye Naibu Waziri Mkuu, akihusika na uratibu wa shughuli za serikali, pia anakuwa waziri mpya wa Nishati.
Mara ya mwisho wadhifa wa Naibu waziri Mkuu ulikuwepo 1995 na kushikwa na Augustin Mrema wakati wa awamu ya pili ya uongozi ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Kwa mara ya kwanza nafasi hiyo ilidumu kwa miaka mitatu (1986 – 1989), ambapo rais wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, alimteua aliyewahi kuwa waziri mkuu katika serikali ya awamu ya kwanza, Salim Ahmed Salim, kushika wadhifa huo.
Mara ya pili, nafasi hiyo iliundwa na Rais Mwinyi, mwaka 1993, baada ya kumteua aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Augustine Mrema, kushika wadhifa huo, ambao alidumu nao mpaka mwaka 1994 kabla hajajiengua kutoka chama cha mapinduzi (CCM). Uteuzi wa leo, unaifanya nafasi hiyo kuundwa nchini kwa mara ya tatu, huku aliyekuwa waziri wa madini Dotto Biteko; akiingia katika historia, kwa kuwa mmoja kati ya watanzania watatu kuwahi kuhudumu katika nafasi hiyo.