WATATU WAHUKUMIWA KUNYONGWA KWA MAUAJI YA JOYCE

Watuhumiwa watatu kati ya wanne wa Kesi ya Mauaji Namba. 29820 ya mwaka 2024 walioshitakiwa kwa kumuuwa Joyce Luhedeka (51), wamehukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Geita adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia, huku Dogan Budeba (44) akiachiliwa huru.

Waliohukumiwa ni Thereza Luhedeka (73) (dada wa marehemu), Mateso Joseph (23) (mtoto wa Thereza Luhedeka) na Elias Galawa (49) (mganga wa kienyeji) wote wakipatikana na hatia ya kula njama na kushiriki mquqji hayo ya Joyce qmbaye alikuwa ni mkazi wa Ikobe, Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita.

Wakili wa Serikali Liberatus Rwabuhanga akiwa na wakili Ipyana Mwantonto na Scholastica Tiffe, wameieleza Mahakama kuwa,Oktoba 11, 2023 washtakiwa walimuua Joyce Luhedeka akiwa nyumbani kwake kwa kumkata na kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake, kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16, rejeo la mwaka 2022).

Wamesema, baada ya kumuua, walizikata sehemu za siri na kutoweka nazo hadi walipokamatwa na kukutwa wakiwa wamezikausha, huku uchunguzi ukibaini sehemu hizo za siri zilikiwa ni za marehemu Joyce Luhedeka na chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.

Hukumu hiyo imesomwa Machi 28, 2025 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fredrick R. Lukuna ambaye amesema Mahakama imezingatia kwa makini na tahadhari kufikia uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka.

Amesema, Mashahidi 16 waliitwa na kutoa ushahidi pamoja na ule wa utetezi na kujiridhisha pasipo kuacha shaka yoyote; washtakiwa watatu walitenda kosa la kumuua Joyce Luhedeka na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *