WATATU WA FAMILIA MOJA MBARONI KWA MAUAJI YA BABA YAO MZAZI

Frank Aman – Geita.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu watatu wa familia moja kwa tuhuma ya Mauaji ya baba yao mzazi aitwaye Hussein Bundala, mwenye umri wa miaka 103 aliyeuawa akiwa nyumbani kwake Februari 05, 2025 majira ya saa 2 usiku katika Kitongoji cha Ihananilo, Kata ya Nyamtukuza Wilaya ya Nyang’hwale kwa kukatwa na kitu chenye makali sehemu za kichwani, usoni na shingoni.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Yombo Hussein Bundala, Mwanamke, Miaka 75; Makame Hussein Bundala, Mwanaume, Miaka 53 na Shija Hussein Bundala, Mwanaume, Miaka 50.

Jeshi la Polisi linakamilisha uchunguzi wa tukio hili kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kiuchunguzi na watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Jeshi la Polisi linalaani vikali vitendo hivi na litahakikisha kila anayeshiriki katika vitendo vya kihalifu anakamatwa na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Katika hatua niingine, Jeshi la Polisi Mkoani Geita Februari 21, 2025 lilitoa taarifa kwa umma kuhusiana na kuwashikilia wanafunzi thelathini (30) wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya Geita iliyopo Manispaa ya Geita kutokana na vitendo vya kufanya vurugu shuleni hapo Februari 20, 2025 majira ya saa 2 usiku.

Jeshi la Polisi limekamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kuwahoji wanafunzi thelathini (30) waliokamatwa Februari 20, 2025 na wengine 41 na kufanya wanafunzi waliohojiwa kuwa sabini na moja (71). Uchunguzi wa tukio hilo umekamilishwa kwa kushirikiana na Bodi ya Shule ya Sekondari ya Geita na tayari hatua zimechukuliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shule dhidi ya wanafunzi sabini na moja (71) waliobainika kuhusika kwenye tukio hilo.

Wanafunzi saba (07) wamefukuzwa Shule ambao ni Laban Manjano aliyelikuwa kiranja mkuu wa Shule hiyo mwaka 2024 alihamasisha mgomo na vurugu hizo, Elias Zacharia, Harrizon Malinga, Ahmed Mashaka, Frank Paulo, Erick Atanga na Alphonce Makelemo.

Aidha, waliosimamishwa shule hadi Mei 05, 2025 ni Wanafunzi 19 na wanafunzi 45 wamesimamishwa shule kwa muda wa siku 21.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *