Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Mwanafunzi Novatus Adelhard Mgeni (15), wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya MT. Kagwa iliyopo Manispaa ya Sumbawanga.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija imeeleza kuwa waliokamatwa ni Pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari MT. Kagwa, Zacharia Mwasenga (47), Walinzi wawili wa shule hiyo Michael Donasio (33) na Geofrey Simon, (30).
Inadaiwa kuwa, Machi 23, 2025 majira ya saa 2:00 usiku watuhumiwa hao watatu walimshambulia Mwanafunzi huyo pamoja na wenzake wawili kwa kuwapiga wakitumia waya, wakiwatuhumu kuruka uzio wa ukuta na kuingia kwenye Mabweni ya Wasichana.

Wanafunzi hao, mara baada ya kushambuliwa walifikishwa kituo cha Polisi Sumbawanga na baadaye kupelekwa Hospitali ya rufaa ya mkoa, ambapo wawili walitibiwa na kuruhusiwa, huku Novatus akihamishiwa Hospitali ya rufaa ya kanda – Mbeya ambako amefariki akiwa anapatiwa matibabu.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limewataka Walimu, Wasimamizi wa Shule na Taasisi za Elimu, kutoa adhabu kwa Wanafunzi kwa mujibu wa taratibu na miongozo iliyotolewa na Wizara ya elimu.