WATANZANIA MSICHOKOZEKE – DKT. SAMIA

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wasikubali kuchokozeka na hatimaye kuivuruga amani ya nchi, katika uchaguzi.

Msingi wa kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, mara kadhaa wenye nia ovu, hutumia nyakati za uchaguzi kuchokozana ili kusababisha vurugu na kuharibu amani ya nchi, akisisitiza Watanzania wasikubali kuchokozeka.

Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Septemba 20, 2025 alipozungumza na wananchi wa Gombani visiwani Pemba, alipokwenda kwa ziara ya kampeni za uchaguzi wa urais.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali yake imejitahidi kusimamia utulivu wa kisiasa, usalama na amani ndani ya nchi.

Katika kipindi hicho, amesema hazikusikika kashikashi zozote, zaidi ya matukio ya ajali na hata waliofanya majaribio ya kuivunja amani walishughulikiwa na kudhibitiwa.

“Niwaombe sana ndugu zangu, kipindi hiki ni kipindi wengine wanakitumia kuchokozana. Niwaombe msichokozeke, msichokozeke kuweni kama mimi mama yenu, dada yenu, bibi yenu, ndugu yenu, nachokozwa sana lakini sichokozeki.

“Kwa hiyo niwaombe sana msichokozeke. Tusivunje amani kwa sababu ya uchaguzi hapana… akiumia mmoja imeumia familia, akiumia mmoja familia yote itahangaika,” amesisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *