
Na Saada Almasi, Simiyu.
Watanzania wametakiwa kujivunia kuendeleza na kuilinda amani iliyopo nchini na kutojihusisha na vitendo vyote vinavyosababisha uvunjifu wa amani ili Taifa liendelee kuwa salama na kuwa kisiwa cha amani Afrika
Hayo yamesemwa na katibu wa halmashauri kuu ya Taifa (NEC),Itikadi ,Uenezi na mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi CPA Amos Makalla, katika maadhimisho ya miaka minne ya Raisi Samia Suluhu Hassan yaliyoandaliwa na viongozi wa chama na serikali mkoani Simiyu na kusisitiza kwamba amani tuliyonayo nchi jirani zinaitamani
“Watanzania kwa ujumla wetu tujitahidi katika kuilinda na kuendeleza amani ya nchi yetu ,tunayo mifano ya nchi jirani ambazo hazina amani na wanaitamani nchi yetu sasa tuendelee kuitunza ili tuzidi kuwa kisiwa cha amani”amesema Makalla
Sambamba na hilo Makala amewataka wananchi kuyaenzi maendeleo ambayo yanafanyika na serikali ya awamu ya sita kwani miradi inakamilika na watanzania wanaitumia
“kuna miradi ambayo hayati Raisi Magufuli aliiacha haijakamilika lakini leo hii reli ya SGR tunaitumia,viwanja vya ndege vinajengwa ,madaraja yanapitika bila kusahau elimu na sekta ya afya na hiyo ndiyo inamfanya Dokta Suluhu Hassan kuwa Raisi bora wa Afrika” – Makala.
Kuhusiana na miradi katika sekta mbalimbali ambayo raisi Samia ameendelea kuitekeleza Makala amesema kuwa katika awamu zote za uongozi zilizopita awamu ya sita ndiyo imetoa fedha za miradi ya maendeleo zaidi na kuwataka watanzania wapuuze maneno yote ya dhihaka kutoka kwa watu wanaoamini serikali haijafanya lolote.
“Awamu ya sita ni awamu iliyotoa fedha nyingi zaidi za kutekeleza miradi ya maendeleo nchini lakini bado wapo wanaobeza na kusema kuwa hakuna kilichofanyika sasa niwaambie wakisema hivyo muwajibu kwa kuwaonyesha kwa vitendo” – ameongeza Makala.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi amesema kuwa hadi sasa pesa nyingi za maendeleo zimetolewa katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na shilingi bilioni 400 za utekelezaji wa mradi wa maji kutoka ziwa Victoria ambayo yanakwenda kumaliza matumizi ya maji ya chumvi mkoani humo.
“Lazima nikiri kwamba kuna fedha nyingi zimeletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya kila mwananchi wa mkoa huu tumepokea zaidi ya Bilioni 400 kwa ajili ya kuvuta maji ya ziwa Victoria ambayo yatakuwa muarobaini wa maji ya chumvi tunayoyatumia hivi sasa kwa nini tusijivunie”amesema Kihongosi.
Naye mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoani humo Shemsa Mohammed amemuomba Raisi Samia atembelee mkoani humo kwani wananchi wako tayari kumpokea kutokana na mengi mazuri aliyoyafanya na kuwafanya wananchi kukosa deni kwake.
“tunaomba utufikishie salamu kwa Raisi Samia kwamba Simiyu tunamuhitaji kwani ameshatembelea mikoa yote kanda ya ziwa lakini isipokuwa Simiyu na sisi kwa aliyoyafanya hatuna deni kwake na tuko tayari kumpokea” – Shemsa