Na Saada Almasi, Maswa – Simiyu.
Wananchi Mkoani Simiyu, wametakiwa kuacha mtazamo hasi juu ya matumizi ya Vyakula na mafuta yaliyoongezwa virutubishi katika familia zao, ili waweze kuondokana na tatizo la udumavu kwa watoto.
Rai hiyo imetolewa baada ya taarifa za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kueleza kiwa lipo tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ambalo linaongezeka huku kati ya watoto 100, kati yao 33 wana udumavu.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Vijiji hivyo vilivyopo Wilayani Maswa Mkoani Simiyu, Afisa kutoka Wizara ya Afya Idara ya Kinga sehemu ya huduma za lishe, Haliye Aboubakar amesema Simiyu ni moja ya Mikoa inayozalisha Vyakula, lakini ni kati ya mikoa ambayo ina lishe isiyofaa kwa watoto na kuwasababishia udumavu.

“Utajiuiliza kwa nini udumavu unaongezeka maana takwimu za mwaka 2016 udumavu ulikuwa asilimia 32 lakini mwaka jana 2024 imefikia hadi asilimia 33.4 wakati huu ni mkoa wenye uzalishaji mkubwa wa chakula tatizo ninini?” amesema Heliye.
Amesema kuwa serikali imeamua kufanya kampeni kwa kushirikiana na sekta binafsi ambayo ni kampuni ya uboreshaji wa lishe (SANCU) ili kuhamasisha lishe bora kwa jamii.
Naye Afisa Lishe Mkoani Simiyu, Dkt. Chacha Magige amesema kuwa wapo baadhi ya wananchi ambao wanaelewa na kutambua umuhimu wa vyakula vilivyoongezewa virutubisho lakini wapo wengine wasioelewa ambao wanapinga na hao ndio chanzo cha huo udumavu.

“Hali ya udumavu mkoani hapa si jambo la kufumbia macho maana kati ya watoto 100 basi 33 wanaudumavu tunatakiwa kuwanusuru hawa watoto,na baadhi yetu tunaelewa na tunatumia vyakula vya virutubishi japo wapo miongoni mwetu ambao wanapinga vyakula hivi na hao ndio wanaleta idadi hii,” amesema Dkt Magige.
Katika ushauri wake, pia amesisitiza chakula cha wanafunzi shuleni na familia kipikwe kwa kutumia unga ulioongezwa virutubisho na kwamba kwa sasa zitafungwa mashine maalum ambazo zitasaidia kuchanganya unga wa mahindi na virutubisho.

Mwakilishi wa Kampuni ya SANCU, Eliamani Mmari amesema kuwa kama Kampuni imejikita katika kuongeza virutubishi katika unga kwa lengo la kuimarisha afya za walaji japo kwa sasa wamebaini watoto walio wengi kuwa na changamoto ya afya kwa kuzaliwa na kasoro kama mgongo wazi,vichwa vikubwa pamoja na mdomo sungura zinazotokana na mama kutopata lishe bora kipindi cha ujauzito
Baadhi ya wakazi wa Vijiji hivyo akiwemo Esther Bashu wa Kijiji cha Mbugamita na Agnes Azami wa Sangamwampuya, wameipongeza serikali kwa kuwafikia huku wakitoa rai kwa elimu hiyo kuwa endelevu kutokana na wanakijiji wengi kutokuwa na ufahamu juu ya vyakula hivyo, hali inayosababisha kuwapa watoto chakula cha aina moja na hivyo kuwasababishia udumavu.