Serikali imesema haitawafumbia macho wale wote ambao wanatumia nafasi zao kuwadhulumu mali wazee ikiwemo mashamba, Mifugo na vitu vingine Kutokana na Uzee wao pamoja na kuwafanyia vitendo vya ukatili.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela wakati akifungua kongamano la Baraza la wazee hapa nchini kuelekea Maadhimisho ya kitaifa ya siku ya wazee Duniani ambayo kitaifa inafanyika Mkoani Geita ambapo amesema kumekuwepo na dhana potofu ya watu kuwadhulumu wazee mali zao hivyo serikali itawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuwanyanyasa wazee hapa nchini.
Akiwasilisha Taarifa ya Wazee wote hapa nchini Mwenyekiti wa baraza la Wazee Taifa Mzee Lameck Sendo ameitaka serikali kuendelea kuongeza kasi katika kutatua kero za wazee hasa katika upatikanaji wa huduma ya afya kwa wazee, Ulinzi pamoja na kuwatambua wazee katika vyombo vya kimaamuzi hapa nchini.
Nao baadhi ya wazee walioshiriki Kongamano hilo wamewataka wazee wote hapa nchini kushirikiana kwa pamoja kukemea mmomonyoko wa maadili unaoendelea kuikumba jamii kila kukicha kwani wao kama wazee wakishirikiana kwa pamoja watajenga kizazi kilicho bora hapa nchini.