WATAALAM WAONYA UHIFADHI WA FEDHA NJE YA MIFUMO RASMI

Wakati shughuli za uchimbaji madini zikiendelea kuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa maelfu ya wananchi mkoani Mara, Wataalamu wa masuala ya fedha wameonya kuwa tabia ya kuhifadhi fedha nje ya mifumo rasmi inaendelea kuwagharimu wachimbaji wengi kiuchumi.

Onyo hilo limetolewa wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT)na kufanyika mjini Musoma,yakilenga kuwajengea wachimbaji uelewa wa namna bora ya kusimamia mapato yao.

Akizungumza katika mafunzo hayo,mkufunzi wa masuala ya fedha kutoka BOT, Mipawa Mipawa amesema wachimbaji wengi hupoteza fedha kutokana na matumizi yasiyo na mpangilio pamoja na kuhifadhi fedha katika mazingira yasiyo salama.

Ameeleza kuwa kutumia mifumo rasmi ya kifedha ikiwemo benki na huduma za kifedha za kidijitali husaidia kulinda fedha, kuweka akiba pamoja na kufungua fursa za uwekezaji.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya fedha kutoka BOT, Kenedy Mwasanga amesema changamoto kubwa si kipato kidogo bali ni ukosefu wa elimu ya namna ya kukisimamia.

“Wachimbaji wengi wanapata fedha nzuri lakini wanakosa mpango wa matumizi na uwekezaji, hali inayowafanya wabaki katika hali ile ile ya kiuchumi,” amesema Mwasanga.

Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gelard Kusaya amewataka wachimbaji kubadili mtazamo na kuanza kutumia taasisi rasmi za kifedha ili kuhakikisha usalama wa fedha zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Amesisitiza kuwa sekta ya madini inaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo iwapo mapato yatatumika kwa tija na kuhifadhiwa kwa usalama.

Baadhi ya wachimbaji walioshiriki mafunzo hayo wamekiri kuwa walikuwa wakihifadhi fedha kwa njia zisizo rasmi, hali iliyowasababishia hasara mara kadhaa, na kueleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kubadilika na kupanga matumizi yao kwa ufanisi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *