WASSIRA AWATAKA WATANZANIA KUITUNZA AMANI YA NCHI.

Na Saada Almasi-Simiyu 

Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania bara, Steven Wassira amewataka watanzania kuitunza na kuithamini amani iliyopo nchini ambayo imedumu tangu ilipoasisiwa na baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wassira ameyasema hayo wilayani Maswa mkoani Simiyu katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la katoliki Parokia ya Nyalikungu akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa amani iliyopo haikuja yenyewe ila kwa kupambaniwa na baba wa taifa hivyo kuitunza ni jukumu la kila mmoja.

“Zipo nchi ambazo hazina amani ni vita na vurugu, ukabila upo kila sehemu udini umeshamiri lakini jiulize kwa nini nchi yetu bado ina amani kwa hiyo tusiichezee jukumu la kuilinda ni la kila mmoja wetu” amesema Wassira.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu Anamringi Macha amewataka waamini hao kushirikiana kwa pamoja katika kuiombea amani ya nchi na rais kwani kusimama kwake ndiko kunakoleta uhai wa amani tuliyonayo.

“Nitashirikiana na nyie katika hatua zote lakini niwaombe tuendelee kumuombea Rais wa nchi yetu kwa sababu bila yeye kusimama na sisi basi Tanzania yenye amani haitokuwepo” amesema Macha.

Naye paroko wa parokia hiyo Deogratius Ntindiko amemshukuru Rais Samia kwa mchango wake katika harambee hiyo ambao utasaidia katika kukamilika kwa ujenzi huo.

Katika harambee hiyo Wassira aliwasilisha kiasi cha shilingi milioni hamsini zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kufanya jumla ya fedha shilingi milioni hamsini na moja na laki nne taslimu pamoja na ahadi ya shilingi milioni 201 na saruji mifuko 105.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *