Wasisitizwa Ufugaji wa Unaokidhi Mahitaji ya Soko Kimataifa

Na Melkizedeck Antony,Mwanza

Mkuu wa mkoa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wafugaji Mkoani humo kuachana na ufugaji wa kienyeji wa mazoea na kufuga kisasa mifugo yao ili wakidhi mahitaji ya soko la nyama kimataifa.

Mhe. Mtanda ametoa wito huo wakati alipotembelea kiwanda cha nyama cha Chobo Investment kilichopo wilayani Misungwi kwa lengo la kujionea uzalishaji na uchakataji nyama unaofanywa na kiwanda hicho.

Amesema Tanzania ina zaidi ya ng’ombe Milioni 40 na ikshika nafasi ya pili kwa ufugaji ng’ombe nyuma ya Ethiopia lakini ni asilimia 5 tu ya mifugo hiyo ndio inafaa kwa uzalishaji nyama hiyo, hali inayopelekea  kutokufanya vizuri katika uchangiaji wa pato la Taifa ambapo kwa sasa ufugaji unachangia kwa asilimia 7 pekee.

Aidha, amempongeza mwekezaji wa Kiwanda hicho kwa kupanua kiwanda  kwa  nyibgeza ya gharama ya dola za kimarekani milioni 3 zaidi kutoka kwenye 10 za awali zilizolenga kuongeza uchakataji wa mazao ya nyama kutoka matumizi ya 47% hadi 100% na kwamba  hatua hiyo itasaidia pia kupatikana kwa bidhaa 153 zinazotokana na  ng’ombe.

Naye, Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. John Chobo amesema kiwanda chao kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 600 kwa saa 8 lakini kwa sasa wanachinja 200 tu huku wakipata mbuzi wachache kutokana na uzalishaji kuwa wa kiwango cha chini na usiokidhi mahitaji.

Amefafanua kuwa ili kufikia malengo ya kupata nyama ya kutosha wameanzisha shamba ambalo wanafuga kisasa, wananenepesha na kuandaa malisho bora kwa mifugo na kuwakaribisha wafugaji kwenda kujifunza ili wazalishe kisasa.

“Kiwanda chetu ni kikubwa na tumekiongezea nguvu hivyo tunatamani kupata ng’ombe wenye uzito mkubwa hadi wa Kilogram 700 kwani mahitaji ya nyama kwenye soko la ndani na nje ni makubwa sana lakini kunakua na uhaba kutokana na ng’ombe wa asili kuwa na uzito mdogo.” Amesema Bwana Chobo.

Vilevile, ametoa wito kwa sekta ya kilimo kuchangia kwenye ukuaji wa sekta ya nyama kwa kuzalisha vifungashio vitokanavyo na zao la pamba linalofanya vizuri nchini (Mutton Cloth) vinavyotumika kuhifadhi nyama kwenda nje ya nchi tofauti na hali ya sasa ambapo vinaagizwa kutoka Vietnam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *