WASIRA AMJIBU ZITTO, WAJITOKEZE WASEME WANATAKA NINI

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amemjibu Kiongozi Mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kuwa CCM haibishani na CHADEMA kwani walisema hawako tayari kupotezewa muda walipotaka kufanya nao mazungumzo.

Wasira ameyasema hayo hii leo machi 30, 2025 katika mkutano wa hadhara mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu na CHADEMA wanatakiwa kujitokeza hadharani ili waseme wanataka nini au waiambie Tume.

Amesema, “mimi niliwaambia tuzungumze Tundu Lissu akasema tutawapotezea muda, sasa mtu ana muda wake na hataki upotee wewe umlazimishe kupoteza muda wake wa nini? Kwa hiyo sisi tunawaambia wakiwa na jambo linazungumzika na linawezekana waje tuzungumze.”

Wasira ameongeza kuwa, “hawataki kuzungumza sasa wanasema hayo mabadiliko wanayoyataka wao ambayo mimi siyajui na hawajapata kuyasema, na leo nataka niwaambie mtuambie mnataka nini hasa maana ‘no reform no refom’ ‘reform’ nini maana ‘tumesha-reform.’

“Watuambie na wawaambie Watanzania kitu gani hasa maana hawasemi sasa na wanachama wao wameanza kuwageuka wao nao wanataka udiwani hata kama sijui wataupata maana kuupata ni majaliwa, lakini unawapa uhuru wa kuongea,” alisema Wasira.

Kuhusu madai ya Zitto Kabwe kwamba CCM imekataa kukaa na CHADEMA, alisema sio kweli kwa kuwa Chama ni mwanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho mwenyekiti wake ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Wasira amefafanua kuwa CCM ni wanachama wa TCD na hiajakataa kikao naLissu.“Akiitisha tutaenda maana sisi ni watu wa amani, hatutaki shari.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *