
Washirika wa mchungaji Paul Makenzie ambaye hivi karibuni alishtakiwa kwa makosa ya ugaidi na mauaji, wameendelea na mgomo wa kula hali ambayo hapo jana iliwawia vigumu kutembea kuingia mahakamani kusikiliza mashtaka dhidi yao.
Wakiwa wamefikishwa katika mahakama moja mjini Mombasa, ili kusikilizwa kwa mashtaka 238 ya mauaji bila kukusudia yanayohusishwa na vifo vya watu zaidi ya 400 katika msitu wa Shakahola, washtakiwa hao walionekana wanyonge na hawakuwa na nguvu ya kutembea.
Washtakiwa hao 95 walisusia kula chakula kwa wiki moja sasa Pia ilikuwa vigumu kwa wao kutembea hadi ndani ya mahakama, hatua iliyomlazimu Hakimu Mkuu wa Mombasa Alex Ithuku kuwatembelea washtakiwa hao katika korokoro ya mahakama, na kuamrisha wote wapelekwe hospitalini kwa matibabu.

Akizungumza mahakamani bila uwepo wa washtakiwa, Wycliffe Makasembo, wakili wa washtakiwa amesema kwamba wateja wake waligoma kula kutokana na imani kwamba kesi hiyo inaweza kuchukua muda mrefu kumalizika na wangeendelea kuteseka mikononi mwa polisi.
Kulingana na upande wa mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mazito na iwapo wataachiliwa kwa dhamana, itakuwa vigumu kuwapata na kuwawasilisha mahakamani.