
Na Saada Almasi -Simiyu
Wanawake wanaojishughulisha na upondaji kokoto maeneo ya Nkololo wilayani Bariadi mkoani Simiyu wameiomba serikali kuwaboreshea mazingira yao ya kazi kwa kuwanunulia mashine ya kupondea kokoto hizo sambamba na kuwarahisishia upatikanaji wa malighafi za biashara hiyo ili biashara yao iwe na tija.
Baadhi yao wamekuwa katika biashara hiyo kwa takribani miaka kumi wakiitegemea kujipatia chakula cha familia sambamba na kupata mahitaji ya Watoto wao huku nguvu kubwa wanayoitumia kupondea kokoto zao ikiwa ni mikono yao.
Akiongea na Jambo FM, Monica Maduhu mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 anayeitegemea kazi hiyo kumtibu mwanae ambaye anachangamoto ya saratani ya kichwa iliyomletea upofu amesema kilio chake kwa sasa ni kwa raisi Dr Samia Suluhu kuwanunulia mashine ya kupondea kokoto ili kazi yao ifanyike kwa urahisi.

“Mimi umri umeenda na hii ndiyo kazi pekee inayonisaidia kupata pesa ya kula na kununua dawa siwezi kulima hata hivi ninavyoponda kokoto naumia kifua,raisi Samia popote ulipo nakuomba utununulie mashine ya kupondea kokoto mikono yangu imechoka” – amesema Monica
Kulwa Mwincheye mmoja wa kina mama hao anasema kuwa ugumu wa Maisha miongoni mwao ndiyo umewafanya kujishughulisha na biashara hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa haina tija ukizingatia trip ya mawe wanaipata kwa gharama kubwa
“Hayo mawe ili yaletwe hadi hapa tunayagharamia shilingi elfu kumi (10) kwa trip moja na bado ukiponda hizo kokoto unaweza kukaa hata mwezi bila kuuza hatuwezi kuacha kwa kuwa maisha ni magumu hatuna kitu kingine cha kufanya” – amesema Kulwa.
Matumaini pekee waliyobaki nayo kina mama hawa ni kilio chao kumfikia raisi wa nchi ili unafuu upatikane kwani licha ya mapambano wanayo yafanya ndoo ya lita kumi ya kokoto wanaiuza kwa shilingi 500 hali inayozidi kuwavunja nguvu ya kazi hiyo.