Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watuhumiwa wanne kwa kosa la kupatikana na silaha bila kuwa na kibali katika Wilaya ya Dodoma mjini na Mpwapwa.
Taarifa ilitolewa na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma hii leo Mei 20, 2024 imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Mei 17, 2025 majira ya Saa kumi kamili jioni katika mtaa wa Kikuyu mission jijini humo, ambapo watuhumiwa wawili wote wakazi wa Kikuyu Mission walikamatwa wakiwa na bastola yenye rangi nyeusi ikiwa na risasi 13 kwenye magazine yake.
“Pia, Mei 19, 2025 majira ya Saa kumi na moja kamili jioni katika mtaa wa Lukole Wilaya ya Mpwapwa walikamatwa watuhumiwa wengine wawili wakiwa na silaha iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za Shortgun iliyokatwa mtutu na kitako
pamoja na risasi tano,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Mei 18, 2025 majira ya Saa nne na dakika 40 usiku katika mtaa wa Mbuyuni kata ya Kizota Jijini Dodoma walikamatwa Nestory Kimario (38) na Thomas Paschal (29), maarufu kwa jina la Sigan wote wakazi wa Mbabala wakiwa na mafuta aina ya diseli lita 2420 yakiwa kwenye madumu 89 yaliyohifadhiwa kwenye gari aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T.273 BKB.
Taarifa hiyo pia imedai kuwa, katika doria na misako inayoendelea limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya kuvunjia, TV sita, Redio saba ambazo ni mali zidhaniwazo kuwa za wizi, pamoja na watuhumiwa 57 wa makosa ya wizi na uvunjaji
“Watuhumiwa 30 wamefikishwa mahakamani na wengine 27 uchunguzi unaendelea.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linatoa wito kwa wananchi wanaomiliki silaha kufuata
taratibu za umiliki halali wa silaha ikiwa pamoja na usalimishaji wa silaha hizo kwa wale wanaomiliki silaha kinyume na taratibu, pia wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu,” ilibainisha taarifa ya Kamanda.