
Maelfu ya waandamanaji wamekusanyika kwa amani siku ya Jumanne asubuhi katika miji mitatu mikuu ya Nigeria kupinga gharama kubwa ya maisha, ambayo imelipuka tangu rais mpya aingie madarakani chini ya mwaka mmoja uliopita.
Huko Lagos (kusini), mji mkuu wa kiuchumi, Abuja (katikati), mji mkuu wa shirikisho, na Kano (kaskazini), jiji la pili kwa watu wengi zaidi nchini, Wanigeria elfu kadhaa waliingia mitaani kwa wito wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi, Nigeria Labour Congress (NLC), kushutumu mageuzi ya Rais Bola Ahmed Tinubu, ambayo yamesababisha mlipuko wa gharama ya maisha.
Alipoingia madarakani Mei 2023, Rais Bola Tinubu alikomesha ruzuku ya mafuta na udhibiti wa sarafu, na kusababisha kupanda mara tatu kwa bei ya petroli na kupanda kwa gharama ya maisha, naira kupoteza thamani yake kwa kasi dhidi ya dola.
Kiwango cha mfumuko wa bei nchini humo kilikaribia asilimia 30 mwezi Januari na maandamano kadhaa tayari yamefanyika tangu mwanzoni mwa mwezi wa Februari katika miji midogo midogo kaskazini na katikati mwa nchi.
Rais wa Nigeria amerudia kuwataka wakazi kuwa na subira, akibainisha kwamba mageuzi yake ya kiuchumi yatawavutia wawekezaji wa kigeni na kufufua uchumi, lakini matokeo chanya ya mageuzi haya ni yanachelewa kuonekana.