Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakata watuhuhumiwa watatu ambao ni wanawake raia wa Burundi kwa tuhuma za kuiba simu 61 katika maeneo tofauti ikiwemo Buhongwa jijini Mwanza na katika Wilaya za Kahama na Shinyanga,ikiwa ni pamoja na kuwalaghai wanaume na kuingia nao katika mahusiano ambapo wanapokwenda faragha huwaibia simu zao na kukimbia,baadaye hupeleka simu hizo nchini Burundi kwa ajili ya kuziuza.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP, Janeth Magomi amesema tayari wanawake hao wameutaja mtandao wanaoshirikiana nao ,ambao uko Burundi na tayari jeshi hilo limeshatoa taarifa katika jeshi la uhamiaji kwa ajili ya taratibu za kisheria kwani wanawake hao wameingia nchini bila kufuata utaratibu.
Aidha jeshi la polisi limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya kupigia ramli chonganishi ambavyo ni mikia 8 idhaniwayo kuwa ni ya ,mnyama aina ya nyumbu na kipande kimoja cha ngozi ya mnyama kidhaniwacho kuwa ni cha simba ,pamoja na mafuta ya dizeli lita 260,na lita 173 ya pombe ya moshi ,vyuma 9 vya kuchimbia visima pamoja na difu ya gari aina ya Toyota Hiace pamoja na noti bandia zenye thamani ya shilingi 85,000.
Katika hatua nyingie jeshi hilo limetoa wito kwa wanachi katika mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuendelea kuimarisha usalama wa mkoa ikiwa ni pamoja na wazazi na walezi kuwa makini na watoto pamoja na kufuatilia mienendo yao katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.