Wanawake wajasiriamali Nchini, wametakiwa kutokukata tamaa mapema kwenye biashara, kwani kufanya hivyo ni kudhohofisha ufikiaji wa malengo yao waliyojiwekea.
Akizungumza katika msimu wa pili wa Chanuo, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kizumbi Trading Company cha mjini Shinyanga, Thekla Mongela amesema mafanikio yake yametokana na uthubutu mkubwa aliokuwa nao licha ya kukutana na changamoto mbalimbali za uendeshaji.
Amesema katika safari ya mafanikio yake alianza kulima mahindi mwaka 1998 akiwa na hekari tatu na baada ya mavuno aliuza mazao hayo ili kupata fedha ambazo aliweka akiba kwa ajili ya kufungua mashine ya nafaka.

“Nilitamani sana kuona nafanikiwa kama mwanamke licha ya wakati mwingine kupata mavuno kidogo hali hiyo haikunifanya nikate tamaa kabisa niliendelea kupambana licha kukatishwa tamaa na watu wachache,” alisema Thekla.
Ameongeza kuwa, juhudi na uvumilivu wa miaka 18 ulimfikisha katika kufikia malengo yake ambapo mwaka 2016 alifungua mashine ya kusaga na kukoboa nafaka iliyompa nguvu zaidi ya kuwa na kiwanda cha unga wa mahindi wa sembe na dona.
Thekla amesema amepata mafanikio makubwa kama mwanamke katika biashara yake ambayo inamfanya kuendesha maisha yake ya kila siku licha ya biashara hiyo kuwa ni ngumu kutokana na hali ya uchumi ilivyo hivi sasa.
Ametaja changamoto ambayo anakutakana nayo katika biashara kuwa nikukosa soko la uhakika na pia wateja kutaka bidhaa kwa bei ndogo.
“Sisi Shinyanga hatuna masoko ya uhakika lakini pia unga wangu uko katika kifungashio nimefuata taratibu zote na kodi nalipa sasa bei haiwezi kuwa ya kawaida mteja mwingine nafuata kwenye bei ndogo ili familia ipate riziki bila kujali ubora wa bidhaa,” ameongeza Thekla.
Aidha ameuelezea msimu wa kwanza wa chanuo wa mwaka 2024 ambao alishiriki kuwa ulimjengea ujasiri wa biashara na kuona fursa nyingine za kibiashara ambazo anazitumia hadi hivi sasa katika kuongeza ubora na ubunifu katika bidhaa zake.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wanawake wajasiriamli kushiriki katika makongamano kama Chanuo katika kutangaza biashara na kutafuta fursa mpya na kuwataka wanawake kuungana na kushikamana katika biashara ili kufikia malengo na kuondokana na utegemezi.