Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
MwenyekitiI wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani Shinyanga, Dkt. Regina Malima amewaasa wanawake kuboresha malezi ya watoto katika familia zao hata ikiwa wanajishughulisha na kujipatia kipato sambamba na kuheshimu juhudi za wanaume kama vichwa vya familia kwani kufanya hivyo kunachangia amani, haki, usawa na maendeleo katika familia na jamii kwa ujumla.
Dkt. Regina ameyabainisha hayo wakati akifungua Kongamano la Wanawake kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoani Shinyanga yanayoadhimishwa Kata ya Bugarama Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, ambapo pia amewasisitiza wanawake wote kuchukua kwa uzito Kaulimbiu hii kwani imebeba majukumu muhimu ya wanawake katika Taifa.

“Ninawaasa wanawake wenzangu kuwa walezi wazuri katika familia licha ya kwamba baadhi yetu tunafanya shughuli za kujiingizia kipato lakini ni wajibu wetu kuitunza familia pamoja na kuheshimu juhudi za wanaume kama vichwa vya familia kwani kufanya hivyo kunachangia amani, haki, usawa na maendeleo katika familia zetu na jamii kwa ujumla,” alisema Dkt. Regina.
Akielezea lengo la kongamano hilo , Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson amesema kuwa kupitia kongamano hilo wanawake watapata fursa ya kupewa elimu zitakazotolewa ikiwemo ya uongozi, uchumi na malezi.

Amesema lengo la elimu zitakazotolewa ni kuimarisha jamii yenye haki, usawa na uwezeshaji, lakini pia elimu hii itaendelea kutolewa kwa muda wote hata baada ya maadhimisho kuhitimishwa.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii mkoani Shinyanga, Lydia Kwesigabo ameelezea kuhusu Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM).

Aidha, amewasihi wazazi na walezi kuwalinda watoto dhidi ya mazingira yanayopelekea ukatili kwani husababisha changamoto za afya ya akili kwa watoto hivyo wazazi wana wajibu wa kulinda ulinzi na usalama kwa watoto wao.
Mkoa wa Shinyanga unaadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani leo tarehe 6 Machi, 2025 ambapo mgeni rasmi atakuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.