WANAWAKE 92 WAPOTEZA MAISHA KWA CHANGAMOTO ZA UJAUZITO – DKT. MOLLEL

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2024, wanawake 92 walipoteza maisha kutokana na changamoto mbalimbali zilizosababishwa na kuharibika kwa mimba.

Dkt. Mollel ameyasema hayo leo Januari 31, 2025 Bungeni hapa Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mhe. Fatma Toufiq aliyehoji ni Watoto wa kike wangapi na Wanawake wangapi walioathirika na utoaji mimba usio salama nchini. 

“Kwa mwaka 2024 idadi ya wanawake na wasichana waliopata changamoto ya kuharibikiwa na mimba na kupata huduma katika vituo vya huduma za Afya ni kama ifuatavyo, Wanawake na wasichana 181,071 ambao walipatiwa huduma na kuruhusiwa kama wagonjwa wa nje (outpatients).

Wanawake na Wasichana 32,512 ambao walipatiwa huduma wakiwa wamelazwa (inpatients),”amesema.

Aidha akijibu swali la nyongeza la Mhe. Toufiq kuhusiana na wanawake wanaobakwa na kukubwa na kadhia hiyo Dkt. Mollel amesema suala hilo linahitaji elimu zaidi ya kisaikolojia baada ya kutokea na wao kulinda maovu kama hayo yasiendelee kutokea katika jamii.

Kwa upande wake Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniania (IPU), Dkt. Tulia Ackson amesema kwenye eneo hilo wao kama wawakilishi wa wananchi inabidi wapeleke ombi kwa Serikali ili wafanye mafunzo maalum kwani utoaji wa mimba nchini bado ni kosa la jinai.

“Sasa pamoja na kwamba ni kosa la jinai lakini sasa bado kuna hizo changamoto hizo ambazo zinajitokeza kwa wale wanaotoa mimba na wale ambao mimba zinatoka, sisi ndio tunaotunga sheria lakini ni vizuri tukawa na uelewa mpana juu ya eneo hili kabla hatujaanza kushauri kama sheria pengine tubadilishe kwenye maeneo gani,”amesema.

Amesema kuwa watafanya utaratibu wapate nafasi ya kujifunza na wakisha wasikia wataalam wa afya ili waweze kuwashauri wale wanao wawakilisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *