
Na Saada Almasi -Bariadi,Simiyu
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Fadhili Maganya amewaonya wanasiasa nchini kuacha tabia ya kuchafuana wao kwa wao na kisha kuwahusisha viongozi wa kitaifa kwani kwa kufanya hivto kunaathiri chama na utu wao.

Maganya ametoa onyo hilo mjini Bariadi mkoani Simiyu alipokuwa akizungumza na waombolezaji waliojitokeza kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi CCM mkoa wa Simiyu Jackson Masunga Yuma aliyefariki nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Sasa tuko kwenye kipindi cha uchaguzi na umeibuka mtindo wa sisi wanasiasa kuanza kuchafuana japokuwa sijasikia hapa Simiyu lakini tambueni kwamba majina ya wagombea yatachujwa na atabaki mmoja atakayechuana na mgombea wa chama cha upinzani kama kitakuwepo,sasa umeanza kuchafuana na kutujumuisha sisi viongozi niwaambie hizi nafasi anazitoa Mungu utamchafua mwenzako halafu Mungu anamsafisha hadi utashangaa” amesema Fadhili.

Sambamba na hilo Maganya ameitaka familia ya marehemu Jackson Muya kudumu katika yote mema aliyoyafanya mpendwa wao huku wakiyaenzi na kuyatenda kamna njema ya kumuenzi katika Maisha yake ya milele.

Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed amewataka wanaccm mkoani humo kutothamini vyeo vya duniani na kusahau akhera yao kwani unapofika muda yote hubaki isipokuwa matendo mema na utu waliokuwa nao duniani
“Niwatake wana CCM wote tusithamini vyeo tukasahau utu na kutendeana mema kwani unapofikia muda kila kitu tutakiacha na kuondoka bila chochote, mzee wangu Jackson Yuma aliniaga akienda kutibiwa India na kuniahidi kwamba akirudi tutaendelea kukipambania chama lakini badala yake amerudishwa kwenye sanduku,hili linauma sana “amesema Shemsa
Aidha mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Simiyu Njalu Silanga amesema kuwa yapo mengi ya kumkumbuka mzee Yuma ikiwa ni pamoja na kuwalea Watoto wake 39 licha ya kuwa hakusoma alichukua maamuzi ya kujenga shule ili Watoto wake na watu wake wa karibu wapate elimu ambayo yeye hakuipata hivyo kwa wema huo kila mtu anapaswa kujifunza
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu Anamringi Macha amewapongeza wananchi wa mkoa huo kwa ushirikiano waliouonyesha huku akiwataka kuendelea kuyaishi maono na matendo mema aliyokuwa akiyafanya mpendwa wao
Marehemu Jackson Masunga Yuma amehudumu katika nafasi ya uenyekiti wa jumuiya wazazi mkoa hadi umauti unamfika ambapo pia ameacha mke na Watoto 39 pamoja na wajukuu kadhaa