Na Adam Msafiri, Butiama – Mara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri ameagiza wanasayansi, watafiti na wataalamu wa ikolojia kutoka Tanzania na Kenya kushirikiana kikamilifu katika kutafuta suluhu endelevu za changamoto za uhifadhi wa Bonde la Mto Mara.
Amesema mfumo wa ikolojia wa bonde hilo ni uti wa mgongo wa rasilimali maji, bioanuai, na maisha ya vizazi vijavyo.

Akizungumza katika Kongamano la Kisayansi la Bonde la Mto Mara lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, Butiama, Mhandisi Waziri amesema,
“Kongamano hili linatoa fursa ya kubainisha na kujadili maarifa ya kisayansi kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za Bonde la Mto Mara yakiwemo maji, na malengo mahususi ni pamoja na kuwasilisha matokeo ya tafiti za kisayansi zinazohusu hali ya mazingira ya bonde la Mto Mara, pia kuweza kuwa na mjadala kati ya watafiti,watunga sera,jamii na wadau wengine.”

Kongamano hilo limewaleta pamoja wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Teknolojia,Chuo Kikuu cha Maasai Mara nchini Kenya,pamoja na washiriki kutoka Uganda na Rwanda,hatua inayodhimisha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kulinda mfumo wa ikolojia wa Bonde la Mto Mara.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Mto Mara,Dkt Masinde Bwire,ametoa wito kwa serikali ya Tanzania kuongeza jitihada za usimamizi wa sheria zinazohusiana na ulinzi wa vyanzo vya maji.

“Tungependa kuona utekelezaji wa sheria hizo hasa katika eneo la kutunza ile mita 60 kutoka chanzo cha maji. Mfano wenzetu Kenya wamejenga uzio wa umeme kuzuia uharibifu katika Msitu wa Mau,na sisi Tanzania tuone mfano huo na tuweke jitihada katika uhifadhi wa mazingira na mito.” Amesema Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, David Ole Sankok.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa mto Mara unalindwa ipasavyo kwani hauzifaidishi nchi za Tanzania na Kenya pekee,bali pia mataifa mengine Afrika.”

Mara Day, ambayo imeanza Septemba 12, 2025 na kuhitimishwa Septemba 15, 2025 imejumuisha mfululizo wa shughuli ikiwemo upandaji miti, kongamano la kisayansi na hafla fupi ya kuwakilisha wageni kutoka nchi jirani.


