Na. Irene Kishiwa – Chumba cha Habari.
Serikali Nchini, imesema itawachukulia hatua kali wote wanaoingia katika migogoro ya mapenzi, kukimbia mimba, kutelekeza Wanawake na watoto ili iwe mfano na fundisho utakaosaidia kupunguza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu nchini.
Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi ameyasema hayo hivi karibuni na kuongeza kuwa, Wizara imeandaa muongozo kuona watoto ambao wanaishi katika mazingira hatarishi wanaweza kupatiwa haki zao za msingi uliozingatia uwepo wa sheria ya mtoto sura namba 13 kifungu namba 51B inayowataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wa malezi kwa watoto wao.

“Wazazi na walezi ambao watashindwa ama kukaidi kutimiza wajibu huo watakabiliwa na adhabu ya kutoa faini ya zaidi ya shilingi milioni tano au kifungo si chini ya miezi sita na kisichozidi miaka mitatu na kwamba utaratibu huo upo na ninatoa wito kwa wazazi na walezi wote kote nchini kutimiza majukumu yao kwa watoto wao,” alisema.

Ameongeza kuwa, ugomvi ama umasikini si sababu ya kumuacha mtoto kutangatanga barabarani na kwamba ni bora kuishi na mtoto huyo katika hali na mazingira yote hata kama yawe niya kunywa uji, kula ugali na chumvi kuliko kumuacha na akakosa haki zake za msingi .
Aidha, Mahundi amesema Wizara itaendelea kusimamia nakuhakikisha watoto hao wana pata haki na wazazi pamoja na walezi watakaokwepa kutoa huduma ya matunzo kwa watoto hao, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.



