Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Tanzania imekua na ongezeko kubwa la watu wanao tumia vyoo bora kutoka asilimia 21 mwaka 2016 hadi asilimia 74.8 mwaka 2022 ambapo ni hatua chanya ya kufikia lengo la 6.2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya 2030 “Sustainable Development Goals”.
Waziri Ummy amesema hayo katika tamko lake likionesha hali ya matumizi ya vyoo nchini ambapo mikoa inayoongoza kwa matumizi ya vyoo bora ni Dar es Salaam (98.5%), Ruvuma (92.1%) na Njombe(87.6%).
Aidha, Waziri ummy amesema Licha ya kuwa tumepiga hatua kwenye kiashiria hicho bado kuna baadhi ya watu hawatumii vyoo ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 9.8 ya watu nchini hawana vyoo kabisa ambapo hali ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini.
Hata hivyo Waziri Ummy amebainisha mikoa inayoongoza kwa kutokuwa na vyoo ni Katavi (24.3%), Simiyu (24.3%) na Manyara (22.3%) huku akiagiza Sekretatarieti za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kaya zote nchini zinakuwa na vyoo bora.