Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ametaka wanaobainika kuiba fedha za umma kwenye ripoti ya CAG wanyongwe.
Waitara amesema hayo Bungeni wakati wa mjadala kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo amesema Watanzania wengi wanaishi maisha ya ufukara kiasi cha kushindwa kuwalipia Ada Watoto wao kutokana na Fedha za Umma kufanyiwa Ubadhirifu na Watumishi.
Amesema suala hilo linafanyiwa uzembe na Wabunge kwa kutochukua hatua na kuongeza kuwa “Kama mtu amebainika ameiba na ripoti ipo, taarifa zipo, vyombo vipo, lakini hawajibishwi, je, wanafundisha nini vijana wa Tanzania? Kwamba mtu ataiba na kuhamishwa tu Wizara bila ya kuwajibika?”
Waitara amesema Wabunge wasisubiri kuambiwa
wanatakiwa kuchukua hatua, bali wawawajibishe Watumishi wanaotajwa katika ripoti hizo kwa sababu wao ndiyo wenye dhamana ya kufanya hivyo na kama Ripoti za CAG zitakuwa zinaishia kukaaa Makabatini kila mwaka yeye (Waitara) ataacha kuchangia maoni juu ya ripoti hizo.