Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro, linawashikilia watu wanane kwa tuhuma za mauaji ya Daudi Wilbard Ntuyehabi, ambaye alikuwa ni mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) katika jimbo la Siha.
Tarifa ya Polisi iliyotolewa hii leo Oktoba 8, 2025 imeeleza kuwa, mauaji hayo yametokea Oktoba 7, 2025 majira ya saa 1:30 usiku, katika Kijiji cha Kilingi kilichopo Sanya juu Wilaya ya Siha, Kilimanjaro.
“Tukio la kujichukulia sheria mkononi limetokea baada ya Daudi Wilbard Ntuyehabi (marehemu) kumchoma kwa kisu tumboni Abdul Issa Mohamed mkazi wa Kilingi kata ya Sanya Juu na kusababisha utumbo kutoka nje,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Inadaiwa kuwa, sababu za Abdul Issa Mohamed kuchomwa kwa kisu ni kitendo chake cha kwenda kuamua ugomvi uliozuka kati ya Daudi Wilbard Ntuyehabi (marehemu) na Hamadi Issa Mohamed.




