Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Ikiwa ni siku moja tangu ulimwengu uadhinishe siku ya wapendao, Paroko wa Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, lililopo Ngokolo Jimbo Katoliki la Shinyanga, Richaerd Masunga amewakutanisha wanandoa 70 katika fukwe ya Bwawa la Songwa, iliyopo katika Kata ya Songwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ili kurudia kiapo chao cha ndoa na kuketi pamoja, kujadiliana changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza na wanandoa hao, Fratery Richard Masunga amesema, wanapaswa kuwa na uvumilivu katika maisha yao ya ndoa ikiwa ni pamoja na kuombana misamaha pale mmoja wapo anapomkosea mwingine na kwamba msamaha limekuwa ni daraja madhubuti katika kuhakikisha wana ndoa wanaishi pamoja mpaka kifo kitakapowatenganisha.

Wanandoa hao, pia wametumia jukwaa hilo kupanda miti pembezoni mwa fukwe la bwawa la songwa lengo likiwa ni kutunza mazingira na kuashiria uhai wa viumbe pamoja na kucheza michezo mbalimbali kama vile karata,draft pamoja na uimbaji wa nyimbo za asili.
Miongoni mwa waliohudhuria majadiliano hayo ni pamoja na wanandoa wakongwe waliodumu kwa zaidi ya miaka 45, Peter Tesha na Mkewe Imakulata Anthony ambapo wameainisha siri ya kuishi maisha marefu kwenye ndoa ni kuvumuiliana, kusameheana makosa, kusema asante kwa chochote hata kama ni kidogo na kubwa zaidi ni kumcha mwenye enzi Mungu.

Wanandoa wengi wameendelea kukumbwa na changamoto mbalimbali zinazotishia uthabiti wa ndoa zao, hali inayochangiwa na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na mtindo wa maisha wa sasa.
Miongoni mwa changamoto kubwa zinazotajwa ni ukosefu wa mawasiliano bora, ambapo baadhi ya wanandoa hushindwa kuzungumza kwa uwazi kuhusu hisia, mahitaji na matarajio yao. Hali hii mara nyingi husababisha kutokuelewana na migogoro ya mara kwa mara.

Wadau wa masuala ya familia wanashauri wanandoa kuimarisha mawasiliano, kushirikiana katika kutatua matatizo, na kutafuta ushauri wa kitaalamu pale inapohitajika ili kudumisha amani na mshikamano katika ndoa.
