Wananchi wilayani Bariadi watarajia kuondokana na changamoto ya mawasiliano ya barabara kufikia Septemba mwaka huu

Wakazi wa mtaa wa Matale, Nyasosi na Ngashanda wilayani Bariadi mkoani Simiyu wanatarajia kuondokana na changamoto ya mawasiliano ya barabara husa kipindi cha mvua, baada ya serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) wilayani Bariadi kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja katika mto Ngashanda, lenye gharama ya Shilingi bilioni 1.2 ambalo litaondoa changamoto hiyo ya muda mrefu.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Bariadi Mhandisi Khalid Mang’ola, wakati akizungumza na waandishi wa habari darajani hapo na kueleza kuwa kabla ya msimu wa mvua kuanza daraja hilo litakuwa limeshakamilika na kuanza kutumika.


“Kufikia mwezi wa tisa tutakuwa tumeshakamilisha, naimani wananchi watapita bila tatizo lolote, kuna wanafunzi wanakwenda kusoma upande wa pili na wenyewe watapita bila tatizo lolote, tunaishukuru serikali kwa kutuletea fedha nyingi sana, kwa mwaka huu tu tunajenga madaraja manne.” Amesema Mang’ola.

Kwa upande wake Msimamizi wa mradi huo wa ujenzi wa daraja Mhandisi Charles Njoelo, amesema kwamba ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia sabini na kwamba utakamilika kwa wakati uliopangwa.

“Wananchi watarajie kukabidhiwa mradi mwishoni mwa mwezi wa tisa, mpaka sasa hivi ujenzi upo kwenye asilimia sabini, sabini na tano, tunatarajia kufikia mwezi wa tisa tutakuwa tumefikia asilimia mia moja.” Amesema Njoelo.

Baadhi ya wananchi wanaotarajia kulitumia daraja hilo wameeleza adha wanazopitia kipindi cha mvua, mto huo unapojaa na kukata mawasiliano ya barabara, na namna ambavyo daraja hilo litawasaidia kuondokana na changamoto hiyo pindi litakapokamilika.

“Kipindi cha mvua usafiri wa gari, wa pikipiki au usafiri wowote tu kuelekea kijijini ilikuwa ni hamna, akina mama wajawazito walikuwa wanajifungulia nyumbani utokana na kukosa usafiri, wengine wanapoteza uhai, watoto wanapoteza uhai wanafunzi hawaendi shuleni, tunaishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hili.”Amesema Spilidioni Honorati ambaye ni mmoja wa wakazi wa Ngashanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *