WANANCHI WA TITYE KASULU WAANZA UJENZI SHULE MPYA YA MSINGI

Na Tryphone Odace, Kasulu – Kigoma.

Wananchi wa Kijiji cha Titye, Kata ya Titye, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wameanza ujenzi wa shule mpya ya msingi ikiwa ni mkakati wa kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya msingi Titye na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.

Ujenzi wa shule hiyo umefikia hatua ya kuweka lenta, huku mradi huo ukiwa umeibuliwa na wananchi wenyewe kwa lengo la kuwaondolea watoto wao changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za elimu.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo, mwakilishi wa Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Respice Swetu, aliwapongeza wananchi wa Kata ya Titye kwa namna wanavyoshiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta ya elimu.

Alisema juhudi zinazofanywa na wananchi hao ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya jamii na serikali katika kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira rafiki na salama.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Titye, Dunia Miheza, alisema wananchi wanaendelea na mikakati ya kuchangishana fedha ili kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unaendelea bila kusimama.

Aidha aliwaomba Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwa kutoa usaidizi utakaowezesha ujenzi wa shule hiyo kukamilika kwa wakati.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Titye, Jeremia Balo, walisema hadi sasa jumla ya shilingi milioni saba zimetumika katika ujenzi wa mradi huo.

Amesema baada ya kukamilisha hatua zilizopo, wananchi wanakusudia kuanza ujenzi wa vyoo kwa ajili ya wanafunzi pamoja na walimu, ili kuhakikisha shule hiyo inakuwa na miundombinu muhimu kwa ajili ya mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Titye waliahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wao katika kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta ya elimu, ili kuboresha huduma kwa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *