WANANCHI WA NZEGA CHANGAMKIENI FURSA ZA KIUCHUMI – MAJALIWA

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora wamehimizwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza baada ya kukamilika na kuzinduliwa kwa Kituo cha mabasi cha Nzega Mjini, kutokana na jiografia ya Nzega Mjini kuwa na makutano ya barabara nyingi muhimu zenye kuunganisha Nchi na Nchi nyingine za jirani ikiwemo Burundi, Rwanda, Congo na Uganda.

Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, leo Machi 12, 2025 wakati akizindua kituo cha Mabasi cha Nzega Mjini, akitoa wito pia kwa Maafisa biashara na Maafisa uchumi wa wilaya ya Nzega kuwasaidia wananchi kutambua fursa zilizopo pamoja na kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya wananchi kuweza kunufaika kikamilifu na fursa hizo ikiwemo ujenzi wa nyumba za kulala wageni, migahawa na hoteli kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu.

Ameitaka pia Halmashauri ya Nzega kuongeza vibanda vya wajasiriamali na wafanyabiashara ndogondogo kwenye kituo hicho cha mabasi alichokizindua mapema leo, akisema ujenzi wa vibanda hivyo utaongeza fursa za ajira kwa vijana wa Wilaya hiyo pamoja na kuchangia ongezeko la mapato kwa serikali kutoka Bilioni 3 za sasa zinazokusanywa na Halmashauri hiyo kwa mwaka na kufikia zaidi ya Bilioni 4.

Akizungumzia Faida za ujenzi wa Kituo hicho cha mabasi kilichojengwa nje kidogo ya Mji wa Nzega, Mhe. Majaliwa amesema mbali ya kurahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji, kujengwa kwa kituo hicho nje ya Mji kumeutanua Mji wa Nzega na kuongeza thamani ya ardhi kwa vijiji vinavyokizinguka kituo hicho kwa pande zote, akitoa wito kwa Halmashauri kuwaongoza wananchi katika upimaji wa ardhi hizo na kuwapatia hatimiliki kama sehemu ya ulinzi na ongezaji wa thamani za ardhi hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *