
Na Saada Almasi-Simiyu
Wananchi mkoani Simiyu wameitaka serikali kuwapatia suluhisho la kudumu la tatizo la kukatika katika kwa umeme kwani imekuwa ikirudisha nyuma harakati zao za utafutaji kwa kuwatia hasara.
Wakizungumza na Jambo FM kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa vyombo vinavyotumia umeme vimekuwa vikiharibika mara kwa mara kwa kupigwa shoti ya umeme pale unapokatika na kurudi ghafla
Arnold Mussa fundi wa vifaa vya umeme wilayani Bariadi amekuwa akikutana na changamoto hiyo ambaye ameiomba mamlaka husika kuchukua hatua ili kuokoa mtaji wake
“Tunaletewa vitu vikiwa vibovu na wateja wetu lakini sasa pale unapokuwa unatengeneza lazima utumie umeme, kuna wakati unafanya majaribio ya kifaa cha mtu kinapiga shoti tena tatizo linaongezeka na kwa kuwa kimeharibikia kwako unajikuta umegharamika tena kwa matengenezo na vifaa” amesema Arnold
Si mafundi pekee wanaopata adha hiyo bali wapo mama lishe ambao wanaandaa vuakula na vinywaji ambayo vikikosa kuhifadhiwa kwenye jokofu huharibika na kuwatia hasara.
Mmoja wa mama lishe Maria Maduhu anasema kuwa amewahi kumwaga sharubati (Juice)aliyokuwa ameiandaa kwa ajili ya wateja wake kuchacha kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo kwa siku nzima
“Imewahi kunitokea nikachachisha juisi sasa ningefanyeje siwezi kuuza ikiwa imechacha ila hiyo siku umeme haukuwepo tangu asubuhi kwa hiyo nikapata hasara” amesema Maria
Kufuatia malalamiko hayo Jambo FM ikafanya jitihada za kumtafuta mkuu wa mkoa huo Kenani Kihongosi ambaye amewahakikishia wananchi tatizo hilo limekwisha patiwa ufumbuzi wa kujengwa kwa kituo cha kupozea umeme.
“Ni kweli tatizo hilo lipo na lililkuwa ni kero kubwa kwa kuwa hatukuwa tumeunganishwa kwenye fridi ya taifa lakini kwa sasa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania umetupatia zaidi ya bilioni 90 ambazo zinakwenda kutumika kujenga kituo kikuwa cha kupozea umeme na kuondoa kabisa tatizo hili” amesema Kihongosi