‘WANANCHI SHIRIKISHENI TRA KUFICHUA BIASHARA ZA MAGENDO’ – KAMISHNA MWENDA.

Wananchi mkoani Mwanza na kanda ya ziwa kwa ujumla wametakiwa kujiepusha na biashara za magendo ambazo zimekua zikifanywa maeneo ya majini kwani ni biashara ambazo zinaathiri uchumi wa taifa.

Rai hiyo imetolewa na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda wakati hafla ya uzinduzi wa boti za kisasa za Kuzuia biashara za magendo ndani ya ziwa Victoria ambapo amesema serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha wanazuia na Kupambana na biashara za magendo zinazofanyika majini kwa maana biashara hizo zina athiri uchumi na kuhujumu biashara zingine ndani ya nchi.

“Biashara za magendo zianathiri uchumi wetu lakini pia zinahujumu biashara nyingine na tunaposema tunatenda haki lazima tuhakikishe hakuna mtu mmoja anapata faida kuliko mtu mwingine, lakini pia biashara za magendo zinaathiri usalama wa nchi yetu pia zikichochea uhalifu , Hivyo wito wangu kwa wananchi niwaombe sana washirikiane na TRA katika kutupa taarifa za wanaoingiza magendo”

Katika hatua nyingine Yusuph pia amesema biashara za magendo kwa kiasi kikubwa ndio zimekua chanzo cha rushwa kwani wafanyabiashara wengi wanaouza bidhaa hizo ndio wanaongoza kwa kuwarubuni baadhi ya watumishi wa serikali hivyo kama serikali wamejipanga kupambana na uuzaji wa mali za magendo.

Aidha pia amesema kwa nchi nzima zipo boti za kisasa saba za kuzuia biashara za magendo ambazo zipo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Tanga, Dar es salaam na nyingine ambayo bado inaendelea kutengenezwa ambayo itapelekwa katika mkoa wa kigoma.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa fedha Hamad Chande akawataka wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kujiepusha na ubebaji wa bidhaa hizo kwani endapo chombo chochote kitabainika au kukamatwa na bidhaa pamoja na mali za magendo basi chombo hicho kitataifishwa na serikali bila huruma yoyote.

”Nawataka wamiliki wa vyombo vinavyotumika kusafirisha magendo ikiwa ni pamoja na mitumbwi,maboti, magari ya aina mbalimbali,pikipiki pamoja na baiskeli kuelewa kua vyombo hivyo vitataifishwa pale itakapotokea kukutwa vimebeba bidhaa za magendo ambazo zio halali”

Hamad pia amesema jukumu la ulinzi dhidi ya bidhaa za magendo ni jukumu la kila mtanzania kwani endapo bidhaa hizo zitaingia hapa nchini zitakwenda kuumiza Taifa zima na siyo mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kama wengi wanavyodhani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *