WANANCHI SERENGETI WAIOMBA SERIKALI KUBORESHA BARABARA.

Na Adam Msafiri, Serengeti-Mara.

Baadhi ya wakazi katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara, wameiomba serikali kuboresha miundombinu kwenye mji huo ikiwemo barabara,hali itakayosaidia kurahisisha shughuli za za kila siku za wananchi zikiwemo za kiuchumi na kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo ya watu.

Aidha wakizungumza na Jambo FM Julai 01, 2025 wamesema kuwa hadhi ya mji wa Mugumu, licha ya kuzungukwa na fursa nyingi ikiwemo Utalii kutokana na uwepo wa Hifadhi kubwa ya Taifa ya Serengeti,lakini bado maisha ya wakazi wa eneo hilo sio ya kuridhishi.

Bwana Samwel Chacha ambaye ni mmoja wa wakazi wa mji huo ameeleza kuwa”Tukizungumzia Serengeti tunazungumzia wilaya yenye jina kubwa sana Duniani,lakini ukiingalia Serengeti ambayo wanakuja kutalii na kuitazama kwa kweli inatia aibu sana”.

Kwa upande wake Daud Zungu amebainisha kuwa kukosekana kwa miundombinu bora ya barabara zinazoingia na kutoka katika wilaya hiyo na mji wa Mugumu,kumekuwa kikwazo katika ukuaji wa mji huo huku akiiomba serikali na mamlaka husika kutumia jicho wilaya hiyo hiyo ili iweze kufunguka katika mtandao wa barabara na kukuza uchumi wa wakazi na wilaya kwa ujumla.

“Unajua Mugumu ipo kisiwa,kwa maana kwamba hakuna barabara ambazo zinatoka,kwahiyo kama kungekuwa na barabara ambazo zimefunguka kama hiyo barabara ya kwenda Arusha maana yake kungechochea kuleta maendeleo”.Amesema Bw.Zungu.

Aidha kuhusu sula la ubovu na uchakavu wa miundombinu ya barabara zilizopo,Meneja wa Wakala wa barabara mijini na Vijijini(Tarura) wilaya ya Serengeti Bw.Frank Mushi ametoa ufafanuzi akieleza kwamba kwa sasa wapo katika hatua za kutangaza zabuni za mwaka wa fedha 2025/2026 na kwamba barabara zote zilizoathiriwa na mvua zitafanyiwa matengenezo.

“Ifahamike tu kwa sasa tupo kwenye hatua za kutangaza zabuni za mwaka wa fedha 2025/2026,hivyo niwatoe wasiwasi wananchi kuwa maeneo ya barabara zote ambazo ziliathiriwa vibaya na mvua,tutazifanyia marekebisho kikamilifu”.Ni kauli ya Frank Mushi,Meneja Tarura wilaya ya Serengeti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *