
Na Saada Almasi – Simiyu
Wakazi wa kata ya Mwaubingi wilayani Bariadi mkoani Simiyu wameiomba serikali kupandisha hadhi zahanati ya Gasuma inayotumiwa na wakazi hao kuwa kituo cha afya ili kiweze kuhudumia wagonjwa kwa ufanisi zaidi
Ombi hilo limetolewa wakati wa mkutano wa hadhara ulioitishwa na mbunge wa jimbo hilo na Naibu Waziri wa maji mhandisi Andrea Kundo Methew wakati wa utoaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi katika jimbo hilo.
Wananchi hao wamesema kuwa kwa sasa zahanati hiyo imekuwa ikuhudumia wanawake zaidi ya 10 wakijifungua kwa siku huku baadhi yao wakihitaji upasuaji.

“Hii ni zahanati ambayo inahudumia wagonjwa wengi wakiwemo akina mama wanaojifungua zaidi ya 10 kwa siku moja na wengine wanahitaji upasuaji wa haraka ,vyumba havitoshi kwa hiyo tunaomba ipandishwe hadhi ili huduma ziboreshe madaktari waongezeke na miundombinu maana sasa wakazi tunaongezeka”Richard Kibiriti diwani wa kata ya Mwaubingi
Naye Amos Makeja mkazi wa kijiji jirani cha Benemhi amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na maboresho ya huduma za afya kwa kuwasogezea zahanati lakini mahitaji yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu
” miaka ya nyuma hatukuwa hivi zahanati na vituo vya afya vilikuwa vichache lakini sasa tumeona vimejengwa na vinaboreshwa tunaipongeza serikali lakini tukipandishiwa hadhi tutaboreshewa zaidi huduma hasa kwa akina mama” amesema Amos
Akizungumza na wakazi hao mhandisi Kundo amesema kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano kumekuwa na mabboresho makubwa katika huduma za kijamii na amedhamiria kuendelea kuweka miundombinu sahihi ili kila mtanzania anufaike nayo
“Mtakumbuka hapa miaka mitano iliyopita hakukuwa na mabadiliko kama niliyofanya katika uongozi wangu na niwahakikidhie nitaendelea kuboresha miundombinu yote ikiwa ni pamoja na kufikisha umeme katika vitongoji 512 na bado nimeunganisha kilomita 573 katika jimbo hili na kuweka moram ili kurahisisha usafiri” amesema Naibu waziri Kundo
Kwa upande wake mjumbe wa baraza kuu la wanawake taifa Tina Chenge amesema kuwa palilpo na maendeleo basi kila mwananchi anatakiwa kujua kuwa yupo mtu aliyewafikiria na kuamua kuyafikisha katika maeneo yao hususan shilingi bilioni 4.1 zilizotolewa na serikali katika miradi ya maendeleo
“Maendeleo yakija mjue kuwa yupo mtu anayewafikiria na kuona haja ya kuwaletea nimeona hapa Raisi kaleta shilingi bilioni 4.1 ya miradi ya maendeleo na tumetimiza mmeyaona, yote ni kwa manufaa yenu” amesema Tina


