
Na William Bundala – Kahama.
Wananchi wa mtaa wa Korogwe kata ya Maalunga wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametishia kufunga barabara ya mtaa wa Korogwe wakishiniza serikali kufanya maboresho ya barabara inayopitisha magari makubwa yanayosomba mchele katika kata ya malunga.

Wakizungumza na Jambo FM wanawanchi hao wamesema kuwa magari makubwa yamekuwa hatari kwa watoto wao wanaosoma katika shule ya Msingi Korogwe baada ya kuacha njia kuu na kupita kando ya shule jambo ambalo ni hatari kwa watoto wao.
“Haya magari awali yalikuwa yanapita barabara ya kule chini ila kwa sasa wanapita kwenye makazi ya watu na mbaya zaidi yanapita kwenye barabara ya ofisi ya kata ya Maalunga kupitia shule ya msingi Korogwe na kanisa la roma ambako kuna watoto wetu wanasoma pale na siku za jumapili kanisa la roma kuna waamumini wengi sasa naona tuifunge tu wasipite ili kuokoa maisha ya watoto wetu” Wamesema wananchi hao.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Korogwe wameiomba serikali kudhibiti magari makubwa yasipite katika barabara ambayo wanavukia na badala yake irekebishe barabara ya awali ili magari hayo yapite kwenye njia yake ili kunusuru ajali kwa wanafunzi hao.
“Hii barabara kwetu sisi ni hatari kwasababu ni ya matumizi yetu sisi ya kupita inabidi wakatazwe kupita barabara hii warudishwe kwenye barabara yao walioyokuwa yanapita,Tungependa kuomba warudishwe kule walikokuwa wanapita ili tuweze kuvuka kwa usalama” Wamesema wanafunzi wa Shule ya Msingi Korogwe.
Kwa upande wao baadhi ya madereva wa magari makubwa wameiambia Jambo Fm kuwa hawawezi kupita kwenye hiyo barabara kwakuwa kuna mashimo makubwa na wanaharibu gari zao mara kwa mara huku wanalipa ushuru mwingi kila wanapoijia mzigo ndio mana wameamua kupita kwenye barabara ya shuleni ili kunusuru magari yao.

“Magari yetu yanaharibika sana kwenye hiyo barabara na kila tunapokuja tunaacha pesa nyingi sana za ushuru,hivi wanashindwa hata kumwaga mawe tuk ama mpango wa kutengeneza barabara hiyo bado ili tuendelee kupita,Kwa sasa tunapita hapa kwenye hii barabara ambayo haijaruhusiwa ili kunusuru magari yasiharibike” Wamesema Madereva hao.
Akizungumza kuhusu tetesi za wananchi kutaka kufunga barabara hiyo Mwenyekiti wa Mtaa wa Korogwe Richard Mbelele amesema kuwa ni kweli wananchi wana hasira na ubovu wa barabara hiyo kwani unasababisha watoto wao kuwa na hofu ya kugogwa pindi wanapokuwa shuleni na kwamba ofisi ya Mkuu wa wilaya,Mkurugenzi na Tarura wana taarifa ya changamoto ya barabara hiyo.
“Ni kweli wananchi wamechoka na ubovu wa barabara hii na wanataka kuifunga kwa sababu ubovu wa barabara hii una hatarisha maisha ya watoto wao wanaosoma shule ya msingi Korogwe,Hizi taarifa viongozi wote wanazo kuanzia ofisi ya mkuu wa wilaya,Mkurugenzi hadi Ofisi ya Tarura” Amesema Mbelele.
Akitoa majibu kuhusu barabara hiyo kwenye kambi ya kusikiliza na kutatua kero ya wananchi iliyoandaliwa na mkuu wa wilaya Mboni Mhita,Mhandisi Masolwa Juma kutoka Wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) amesema kuwa barabara hiyo ipo chini ya mkandarasi na wameshamuelekeza Kwenda kutoa maji kwenye madimbwi na kujaza mawe na kwamba barabara hiyo inatambulika kwa umuhimu wake na muda si mrefu itajazwa kifusi kwasababu ipo kwenye mpango wa matengenezo wa halmashauri.

“Tunatambua umuhimu wa barabara hiyo na ipo chini ya mkandarasi na tumemuagiza akatoe maji kwenye madimbwi na ajaze mawe na baadaye itawekwe kifusi kwani ipo kwenye mpango wa matengenezo ndani ya halmashauri” Amesisitiza Masolwa.