WANANCHI KAHAMA WAJITOLEA KUJENGA BARABARA NA KUCHIMBA MITARO ILI KUJIEPUSHA NA MAFURIKO…

Wakazi wa mtaa wa Sofi, Kata ya Mhongolo, Manispaa ya Kahama, wamechukua hatua ya kujitolea kufanya marekebisho ya barabara inayounganisha Sofi, Mhongolo na Busoka baada ya kukumbwa na changamoto ya mafuriko na ukosefu wa mawasiliano wakati wa masika.

Wananchi hao wameamua kuchangishana michango ya fedha na wengine kujitolea nguvu zao ili kuchimba mtaro na kununua mawe kwa lengo la kuepuka adha za mafuriko zinazozuia mawasiliano Katika eneo hilo.

Neema Toyi yeye ni Mkazi wa Sofi, amesema kuwa barabara hiyo imekuwa kikwazo kikubwa kwao kila mwaka, hasa wakati wa masika ambapo watoto wanashindwa kwenda shule na wamama wajawazito wanapata ugumu wa kufika hospitali.

‘Hii barabara inatutesa sana wakati wa mvua hata kama mvua haitanyesha katika mtaa wetu maji hutoka huko mjini na kutuvamia huku, tunapata shida sana watoto wanashindwa kuvuka kwenda shule, na ukinitazama mimi hapa na hali yangu(mjamzito) ninapata wasiwasi kama nikipata uchungu nitavukaje kwenda hospitali selikali na itutazame itujengee daraja hali ni mbaya sana’ amesema Neema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mhongolo, Emanuel Nangale, amepongeza juhudi za wananchi na kuongeza kuwa wamekuwa wakishirikiana na Tarura kuhakikisha barabara hiyo inapata bajeti.

‘Sisi kama serikali ya mtaa tunatambua tatizo hilo eneo hilo ni korofi sana na tumepambana kuhakikisha barabara inapata bajeti na ikapata bajeti ya serikali kupitia Tarura, Tarura walikuja wakakwangua barabara ila hawajaweka changarawe na daraja ila tumewasiliana na Diwani wa Kata ya Mhongolo amesema analifuatilia kwa karibu’ –  Nangale.

Kwa upande wake Meneja wa Tarura Kahama, Joseph Mkwizu, amesema kuwa barabara hiyo ilikuwa na bajeti katika mwaka wa fedha 2023/2024 na kwamba Diwani ametoa maombi ya kipaumbele kwa eneo la Sofi katika bajeti ya mwaka 2025/2026 ili kutatua changamoto hiyo.

‘Barabara hiyo inayounganisha Mhongolo Sofi na Busoka ilikuwa na bajeti katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo tulijenga kalavati mbili, kuchoronga barabara km 4.7 na kuweka changarawe (moramu) km 1.3 katika eneo la Busoka iliyo gharimu shilingi milion 63’.- Mkwizu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *