
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amesema wananchi 2,400 wanaopisha mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi wataanza kulipwa fidia kuanzia Leo Novemba 16, 2023
Mchengerwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wanaoathiriwa na uendelezaji wa Bonde hilo kwenye eneo la Jangwani jijini Dar es salaam ambapo amesema fidia hiyo inalipwa kwa wananchi wote waliokubali kulipwa na kufanyiwa uhakiki wa taarifa zao za kibenki ili kupisha utekelezaji wa mradi huo na tayari Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha kwa ajili hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila amesema kwa wale wenye malalamiko atawasikiliza na litakalohitaji kupelekwa kwa Waziri atalipeleka.
Naye, Mratibu anayesimamia Miradi inayotekelezwa na Benki ya Dunia, Mhandisi Hamphrey Kanyeye amesema wananchi wa Mitaa 16 watalipwa malipo mbalimbali kutokana na thamani ya vitu walivyonavyo.
“Malipo hayo yatajumuisha kifuta jasho, usumbufu, mali pamoja na kodi ya nyumba ya miaka mitatu kwa wale wananchi waliokuwa na nyumba eneo hilo na wanaishi ili wapate fedha za kulipia kodi ya nyumba kipindi wanaendelea na ujenzi,”amesema.