Serikali imewahakikishia kupata mikopo wanafunzi 226 ambao wameachwa katika ufadhili wa masomo wa Samia ‘Samia Scholarship,’ baada ya kushindwa kukidhi vigezo vya kuendelea kupata ufadhili huo.

Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Omega Ngole amesema litafunguliwa dirisha maalumu la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa ajili yao ili kuwapa nafasi ya kuomba mkopo.
Hata hivyo inaelezwa kuwa, wakati katika ‘Samia Scholarship’ wanafunzi hao walipata ufadhili bure na wa asilimia 100, kupitia HESLB watapata mikopo kulingana na vigezo vilivyowekwa na mfuko huo, huku wakitarajiwa kurejesha kama sheria na kanuni za mfuko huo zinavyoelekeza.