Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mkoa wa Tabora, Mwl. Upendo Rweyemamu, amewataka wadau wa elimu kuhakikisha wanafunzi wanajengewa uwezo wa kujiamini, kueleza changamoto zinazowakabili na kushiriki katika kutafuta suluhisho, hatua inayolenga kuimarisha mazingira salama na yenye usawa katika ujifunzaji.
Mwl. Rweyemamu ametoa wito huo akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Tabora wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wawezeshaji wa Mkoa wa Programu ya TUSEME, yanayofanyika katika ukumbi wa maktaba wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora.

Amesisitiza kuwa kila mdau wa elimu ana wajibu wa kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kusema, kusikilizwa, kujiamini, kushiriki katika uongozi na kuchukua hatua katika masuala yanayohusu maendeleo yao.
Aidha ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na UNICEF imeanzisha Programu ya TUSEME ili kuwawezesha wanafunzi kueleza changamoto wanazokabiliana nazo shuleni na nyumbani, kukuza uwezo wa kujiamini na uongozi hususan kwa wasichana, pamoja na kukabiliana na vikwazo vinavyoweza kuathiri elimu yao, vikiwemo ukatili, ubaguzi wa kijinsia, mimba za utotoni na ndoa za utotoni.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Afisa Taaluma Mkoa wa Tabora, Mwl. Aroon Vedasto, amesema Maafisa Elimu ya Watu Wazima na Maafisa Maendeleo ya Jamii ni kiungo muhimu katika usimamizi wa TUSEME kuanzia ngazi ya halmashauri hadi jamii.
Amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza maarifa na uwezo wao wa kusimamia utekelezaji wa programu, huku akisisitiza umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi kuvunja ukimya na kueleza vikwazo vinavyoathiri ujifunzaji wao.

Kwa upande wake, mwezeshaji kutoka FAWE Tanzania, Bi. Neema Katundu, ameeleza kuwa kuwawezesha watoto kuwa na sauti na kujiamini ni hatua muhimu katika kuwaandalia mazingira bora ya kujifunza.
Programu hiyo pia inalenga kukuza stadi za maisha, usawa wa kijinsia na ushirikiano kati ya wanafunzi, walimu, wazazi na jamii.



