Na Saada Almas – Simiyu.
Wakàzi wa Kata ya Lutubiga Wilayani Busega Mkoani Simiyu, wamejitokeza kuuaga mwili wa Mwanafunzi wa kidato cha pili, Mhoja Maduhu ambaye alifariki baada ya kupewa adhabu iliyopitiliza na Mwalimu wake wa Shule ya Sekondari Mwasamba.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Wanafunzi wenza, wamesema Mhoja na wenzake walipewa adhabu baada ya kushindwa kuwasilisha kazi ya kikundi kwa wakati, lakini adhabu kwa Mhoja iliongezeka baada ya kukwepesha mikono alipokuwa akichapwa fimbo ya kumi.

“Huyu Mwalimu huwa hapendi mtu atoe mikono wakati wa kuchapwa sasa alipotoa Mwalimu alianza kumchapa kichwani na sehemu zingine za mwili, ” anasimulia Paul Ndilanha Mwanafunzi wa darasa hilo.
Paul anaongeza kuwa baada ya Mhoja kuchapwa alipiga hatua chache kisha kuzimia hali iliyomfanya mwalimu kuamuru atolewe nje lakini muda mfupi alizinduka na kuanza kulia ndipo mwalimu huyo akamnyamazisha kwa kumkanyaga kichwani.

“Alimwambia nyamaza halafu akamkanyaga kichwani na kumziba mdomo baada ya hapo alikaa kimya tena wakampeleka chini ya mti lakini tulimuona Mwalimu mwingine anawaita wenzake wakambeba kwenye pikipiki,” anasema Paul
Baba mzazi wa mtoto huyo, Samwel Maduhu anasema walipata taarifa kutoka kwa kaka yake Makoye Maduhu aliyepewa taarifa na Mtendaji wa Kijiji hicho na kumtaka afike Hospitali ya Mkula ambapo baada ya kujua mtoto wao kafariki waliitaka Hospitali hiyo kuwapatia binti yao na kumpeleka Hospitali ya Kanda Bugando, kwa ajili ya uchunguzi.

“uchunguzi ulionyesha mtoto ana majeraha kichwani na kuvuji damu kwenye ubongo, nakemea matukio haya sijui ni kwa nini walimu wanatoa adhabu za kupitiliza kiasi hiki naomba serikali itusaidie kuchunguza hii shule waache kufanya hivi matukio haya yanaumiza,” Samwel Maduhu.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Dwasi Machai amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema si mara ya kwanza kuikanya shule hii kutokana na adhabu kali kwa watoto na kuongeza kuwa mwaka 2024 walimuadhibu mtoto wa kidato cha nne Magwala Ezekiel ambaye alipata ulemavu wa kudumu kwa madhara yaliyopatikana katika uti wa mgongo wake.

“Tulikutana katika kikao pamoja na Wanakijiji wengine tukazungumzia suala la adhabu kali wakasema wataacha na wataomba msamaha kwa familia ya huyo mtoto lakini cha ajabu mwezi uliopita tukio lingine linatokea tena na hadi sasa hili ni tukio la pili la kifo katika familia moja, nakemea tukio hili kwa sababu hata Wanahitaji wanaanza kuigopa kupeleka wanafunzi,” Mwenyekiti Dwasi.
Shule ya Sekondari Mwasamba imejengwa kwa mfumo wa kuhudumia vijiji vinne vya Mwakiloba, Mwangika, Mwasamba na Lutubiga na hadi sasa tayari matukio matatu yameripotiwa kuathiri Wanafunzi kutokana na adhabu zinazopitiliza na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku likimshikilia mtuhumiwa.