WANAFUNZI MAHITAJI MAALUM, WANAOISHI MAZINGIRA HATARISHI UVINZA WAPEWA FARAJA

Na Tryphone Odace, Uvinza – Kigoma.

Wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanaoishi katika mazingira hatarishi kutoka Kata za Ilagala, Buhingu na Kalya Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma, wamepatiwa chakula na vifaa vya masomo kupitia ushirikiano wa Restless Development na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Msaada huo umelenga kuwawezesha wanafunzi hao kuendelea na masomo katika mazingira bora, kupunguza changamoto zinazoweza kuwafanya kuacha shule na hatimaye kuwawezesha kukamilisha elimu yao.

Miongoni mwa misaada iliyotolewa ni magunia 88 ya mahindi, magunia 17 ya maharage, maboksi 188 ya karatasi za limu, maboksi 17 ya kalamu, maboksi 112 ya madaftari madogo pamoja na katoni 31 za madaftari makubwa (counter books).

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Restless Development, Ridhiwani Juma, alisema msaada huo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha watoto na vijana wanapata haki ya elimu bila kujali changamoto wanazokabiliana nazo.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunaunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi” alisema Juma

Alisema kuwa uwepo wa mahitaji muhimu kama chakula na vifaa vya shule ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuwasaidia wanafunzi kuendelea na masomo na kuongeza ari ya kujifunza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Godfrid Nkuba, aliishukuru Restless Development na UNICEF kwa msaada huo, akisema umekuja wakati muhimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Nkuba aliwataka wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Halmashauri katika kuimarisha elimu, hususan kwa watoto wanaokabiliwa na changamoto zinazoweza kuhatarisha safari yao ya kielimu.

“Ni muhimu kuhakikisha watoto hawa wanapata mahitaji muhimu ya msingi ili waweze kubaki shuleni, kujifunza na hatimaye kutimiza ndoto zao,” alisema Nkuba.

Naye Mratibu wa UNICEF Wilaya ya Uvinza, Mwalimu Erick Mhongole, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha mazingira ya elimu nchini.

Mhongole amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha watoto na vijana wanapata mazingira salama, rafiki na wezeshi ya kujifunzia.

Aliongeza kuwa juhudi za pamoja zinapaswa kuendelea ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma kutokana na mazingira magumu ya maisha, ulemavu au changamoto nyingine zinazoweza kuathiri upatikanaji wa elimu.

Msaada huo unatarajiwa kuchangia katika kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kuongeza ari ya kujifunza na kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi kuendelea na masomo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *