
Watu wenye silaha wamewateka zaidi ya wanafunzi 280 kaskazini mwa nchi ya Nigeria kwenye mji wa Kuriga, ambapo mamlaka na mmiliki wa shule ambayo wanafunzi hao walichukuliwa, wamethibitisha.
Hii ni idadi nyingine kubwa zaidi ya wanafunzi kutekwa tangu tukio la mwaka 2021 katika shule ya Chibok, pia kaskazini mwa nchi hiyo.
Licha ya kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, polisi kwenye jimbo la Kaduna, hawajatoa taarifa zaidi katika tukio lililotekelezwa maajira ya asubuhi wakati wanafunzi wakiwa wamemaliza mkutano wa asubuhi.
Hapo awali, mamlaka zilikuwa zimetaja idadi ya wanafunzi waliotekwa kuwa ni zaidi ya 100 lakini mwalimu mkuu wa shule hiyo Sani Abdullahi ameeleza kwamba waliotekwa ni wanafunzi 287.
Utekaji nyara wanafunzi kutoka shule za kaskazini mwa Nigeria umekuwa ni jambo la kawaida na chanzo cha wasiwasi tangu 2014 wakati wanafunzi zaidi ya 200 wa Chibok walipotekwa kwenye jimbo la Borno.
Tayari mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za bindamu, yamezitaka mamlaka za Nigeria kuhakikisha wanafunzi hao wanapatikana, ambapo huenda watekaji wakataka kulipwa kiasi cha fedha ili kuwaachia.