Na Saulo Stephen – Singida.
Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Singida wamekumbushwa kuendelea kuishi na kuzingatia itikadi ya chama hicho inayojikita katika misingi ya demokrasia ya kweli, uwazi, haki na uwajibikaji.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CHADEMA na Mlezi wa Kanda ya Kati, Salma Kasanzu, wakati wa Kikao cha Ndani cha Mashauriano cha CHADEMA Mkoa wa Singida kilichofanyika Septemba 1, 2026.

Kasanzu amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kuendelea kushikamana na misingi ya itikadi ya CHADEMA huku wakijenga ushirikiano na umoja katika utekelezaji wa shughuli za chama.
Mbali na masuala ya itikadi, kikao hicho pia kimejadili umuhimu wa upatikanaji wa Katiba Mpya, huku wajumbe wakibadilishana mawazo kuhusu mustakabali wa taifa na nafasi ya wananchi katika mchakato huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Athumani Omari Toto, amesema chama hicho mkoani humo kipo imara na kinaendelea kutekeleza shughuli zake kwa ushirikiano mkubwa.
Amesema umoja uliopo miongoni mwa viongozi na wanachama ni miongoni mwa mambo yanayokifanya chama hicho kuendelea kuwa imara katika Mkoa wa Singida.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe wa CHADEMA kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Singida, akiwemo Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Samweli Mallo, pamoja na viongozi na wajumbe wengine wa chama hicho.




