Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni Kibamba, amewataka Wamachinga wanaofanya biashara barabarani kuondoka na kurejea katika maeneo rasmi yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya biashara.
Ametoa kauli hiyo wakati akiongoza zoezi la usafi lililofanyika katika eneo la Soko Kuu la Mwanza. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha usafi na utaratibu vinaimarika ndani ya jiji.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Serikali ya Wilaya ya Nyamagana imeelekeza kuhakikisha machinga wote wanaondoka barabarani. Amesema uamuzi huo umelenga kulinda usalama wa wananchi na kuepuka msongamano unaosababishwa na biashara za barabarani.
Ameongeza kuwa viongozi wa serikali na mitaa wamepewa majukumu ya kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo, ili Jiji la Mwanza liwe safi, salama na lenye mpangilio mzuri wa kibiashara.


